'WATENDAJI WA GHALA ZINGATIENI WELEDI, UADILIFU'
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya, amewaelekeza watendaji wa ghala kuzingatia weledi na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha ufanisi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS).
Akifunga mafunzo ya watendaji wa ghala kuelekea msimu wa korosho 2026/27 yaliyoandaliwa na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Mwaipaya amesema maarifa waliyoyapata washiriki yanapaswa kutumika kuboresha usimamizi wa ghala na kuongeza manufaa kwa wakulima na taifa.
Amesisitiza umuhimu wa watendaji hao kusimamia bidhaa kwa uadilifu na kutoa taarifa sahihi kuhusu bidhaa zilizohifadhiwa ghalani ili kuimarisha imani ya wakulima na wadau wengine katika mfumo huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, amesema Bodi hiyo inaendelea kuboresha mfumo na kupanua wigo wa bidhaa zinazouzwa kupitia mfumo huo, ambao kwa sasa unatekelezwa katika mikoa 24 nchini, huku jitihada zikiendelea kuufikisha katika mikoa miwili iliyosalia.
Bw. Bangu amesema mafanikio ya biashara kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala yanahitaji maandalizi, maarifa na maadili ya watendaji, hivyo WRRB itaendelea kuwekeza katika mafunzo na utoaji wa elimu kwa wadau ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha mfumo huo unaleta manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
