BODI YA WAKURUGENZI YA WRRB YAWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WAKE KUFUATIA KUKAMILIKA KWA MUDA WAKE WA KIKAZI
BODI YA WAKURUGENZI YA WRRB YAWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WAKE KUFUATIA KUKAMILIKA KWA MUDA WAKE WA KIKAZI
Dodoma, Oktoba 27, 2025 – Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imewasilisha rasmi taarifa yake ya utekelezaji kufuatia kukamilika kwa muda wake wa kisheria wa uongozi. Hafla ya uwasilishaji wa taarifa hiyo imefanyika katika Ofisi za Wizara ya Viwanda na Biashara zilizoko Mtumba, Dodoma, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara, watendaji wa WRRB na wadau wa sekta ya kilimo.
Akizungumza wakati wa kupokea taarifa hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, ameipongeza Bodi hiyo kwa kazi nzuri iliyofanyika katika kusimamia na kuimarisha mfumo wa stakabadhi za ghala nchini. Amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa mfumo huo kupitia sera thabiti na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya masoko na maghala.
Dkt. Hashil amebainisha pia kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uongozi mahiri wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Said Jafo (Mb), ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mfumo wa stakabadhi za ghala unakuwa chachu ya kukuza biashara, kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha usimamizi wa masoko ya mazao.
Kwa upande wake, Bw. Godwin Mkanwa, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya WRRB, alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Wizara, Bodi na wadau wa sekta ya kilimo. Ameshukuru Wizara kwa kutoa ushirikiano wa karibu katika kipindi chote cha uongozi wao na kwa kuendelea kulisaidia Shirika hilo kufanikisha majukumu yake kwa weledi na ufanisi.
Naye Bw. Asangye Bangu, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, amepongeza Bodi hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kukuza mfumo wa stakabadhi za ghala na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau. Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano chanya kati ya Serikali, taasisi za sekta ya kilimo, na wadau binafsi. Aidha, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha uwekezaji mkubwa katika bidhaa za kilimo na kwa kuendelea kuutangaza mfumo wa stakabadhi za ghala ndani na nje ya nchi.
