TANZANIA YAENDELEA KUFUNGUA SOKO LA MAZAO KIMATAIFA

TANZANIA YAENDELEA KUFUNGUA SOKO LA MAZAO KIMATAIFA
Tanzania inashiriki kwenye Kongamano la Kimataifa la Ufuta na Karanga ambalo mwaka huu linafanyika Jijini Istanbul, Uturuki kuanzia tarehe 5-7 Septemba 2025. Kongamano hilo linajumuisha mataifa yanayolima mazao ya Ufuta na Karanga, wanunuzi na wazalishaji wa zana za kilimo.
Katika Kongamano hilo, ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Ndg. Sempeho Manongi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara katika Wizara ya Viwanda na Biashara, ambaye ameambatana na washiriki kutoka Mamlaka ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX). Ujumbe huo umeelezea hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuleta mageuzi kwenye uzalishaji wa zao la Ufuta na mazao mengine ili kuinua uchumi wa wakulima na nchi kwa ujumla. Vilevile, ujumbe huo ulishiriki mijadala na mikutano ya pembezoni na kampuni mbalimbali kwa lengo la kukuza mtandao wa masoko na kukaribisha wawekezaji na wanunuzi kununua mazao kutoka Tanzania.
Kwa kutambua umuhimu wa kilimo cha ufuta kiuchumi, ujumbe huo ulifanya mazungumzo na washiriki mbalimbali ikiwemo kampuni na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuwavutia wawekezaji, kununua mazao ya wakulima na kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani katika uzalishaji wa mazao.
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania inazalisha takribani tani 300,000 za ufuta, kiasi ambacho kinatarajiwa kuendelea kuongezeka. Kwa ujumla ushiriki wa Tanzania kwenye kongamano hilo umetoa fursa ya kuendelea kunadi sekta ya kilimo Kimataifa hasa kwa kukutana wanunuzi wapya na kampuni zinazokusudia kuwekeza ambapo hatua hii itaongeza mauzo ya ufuta nje ya nchi na mapato ya nchi sanjari na kuinua hali ya wakulima wetu.
Ni wazi kwamba ushiriki wa nchi yetu kwenye Kongamano hilo na mchango wa Ubalozi wa Tanzania uliopo nchini Uturuki kwa kuratibu na kufanikisha ziara hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mikakati ya Serikali hususan diplomasia ya uchumi katika kuleta tija na ushindani kwenye sekta za kimkakati ikiwemo kilimo kupitia ushirikiano na mataifa mengine.