WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA AZINDUA BODI YA WAKURUGENZI YA BODI YA USIMAMIZI WA STAKABADHI ZA GHALA (WRRB)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA AZINDUA BODI YA WAKURUGENZI YA BODI YA USIMAMIZI WA STAKABADHI ZA GHALA (WRRB)
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), leo tarehe 12 Desemba 2025 amezindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Hashil Abdallah, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, pamoja na Prof. Geraldine Rasheli, Mwenyekiti wa Bodi mpya. Pia walikuwepo Bw. Asangye Bangu, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB ambaye pia ni Katibu wa Bodi, wajumbe wa Bodi, wakurugenzi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, wakuu wa taasisi wadau muhimu wa mfumo wa Stakabadhi za Ghala kutoka TMX na TCDC, wawakilishi wa wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, Viongozi wa dini na waandishi wa habari pia walishiriki katika tukio hilo muhimu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mhe. Kapinga aliielekeza Bodi kuhakikisha inaendeleza mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika usimamizi wa mfumo wa stakabadhi za ghala nchini. Alisisitiza kuwa Bodi inapaswa kuwa “Bodi ya Matokeo, si Bodi ya Mchakato”, akitoa wito kwa uongozi mpya kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na ufanisi ili kuboresha zaidi mfumo huo muhimu katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na biashara.
Aidha, aliwataka wajumbe wa Bodi kuimarisha usimamizi, kuongeza uwazi na kuhakikisha mfumo unawanufaisha wakulima, wafanyabiashara na wadau wote nchini. Uzinduzi wa Bodi hiyo unatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa malengo ya WRRB katika kuboresha utendaji wa maghala na kuwezesha sekta ya kilimo na biashara kukua kwa tija. Kwa upande wake Mhe. David Silinde amemwakikishia Mhe Waziri wa Viwanda na Biashara kuwa Wizara yake itaendelea kufanya kazi na Mfumo huu kuhakikisha unafikia mafanikio makubwa kuliko yaliyopo hivi sasa. Akitoa shukrani, Prof Rasheli ameahidi kuwa Bodi yake itayatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa Viongozi hao na kuwa Bodi hii itakuwa ni ya matokeo na sio ya michakato.
