Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
Kamati ya Usaili wa Waendesha Ghala kwa Msimu wa Korosho Yafanyika Mtwara
23 Sep, 2025
Kamati ya Usaili wa Waendesha Ghala kwa Msimu wa Korosho Yafanyika Mtwara

 

Mtwara, 23 Septemba 2025

Kamati ya Usaili wa Waendesha Ghala kwa Msimu wa Korosho Yafanyika Mtwara

Kamati ya usaili wa waendesha ghala kwa msimu wa korosho imeendesha usaili kwa waendesha ghala mkoani Mtwara leo tarehe 23 Septemba 2025. Kamati hiyo inaundwa na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) pamoja na Vyama vya Ushirika.

Lengo kuu la usaili huu ni kuhakikisha kuwa ghala zote zitakazoshiriki katika mfumo wa stakabadhi katika msimu ujao wa korosho zinaendeshwa na wataalamu wenye weledi, uadilifu na uwezo wa kusimamia mfumo kwa ufanisi na uwazi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Bw. Revelian Ngaiza, amesema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya mikakati ya serikali na wadau kuhakikisha mfumo wa stakabadhi za ghala unazidi kuboreshwa kwa manufaa ya wakulima na taifa kwa ujumla.

“Tunaamini kuwa kupitia mchakato huu tutapata waendeshaji ghala wenye uwezo na nidhamu ya kitaaluma, ili kuhakikisha msimu wa korosho unakuwa na tija na uwazi kwa wakulima na wadau wote,” alisema Bw. Ngaiza.

Katibu wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Ndugu Asangye Bangu, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa ghala ili kuongeza ufanisi wa mfumo na kuhakikisha haki ya mkulima inalindwa katika kila hatua.

Hatua hii ni sehemu ya jitihada endelevu za kuboresha mfumo wa stakabadhi za ghala kwa zao la korosho, kuhakikisha kuwa wakulima na wadau wote wa sekta hii wananufaika ipasavyo kupitia usimamizi bora na wa uwazi.

Mwisho