Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
BODI YA USIMAMIZI WA STAKABADHI ZA GHALA YAPONGEZWA KWA UTENDAJI MZURI WA MAJUKUMU YAO
04 Jul, 2022
BODI YA USIMAMIZI WA STAKABADHI ZA GHALA YAPONGEZWA KWA UTENDAJI MZURI WA MAJUKUMU YAO

NAIBU Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb) ameitembelea Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na kuipongeza menejimenti pamoja na watumishi wake na kusikiliza kazi na majukumu ya taasisi pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo.

Katika taarifa yake Mhe. Naibu Waziri ameeleza jinsi taasisi hii ilivyoleta mageuzi ya kiuchumi mara baada ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi (Warehouse Receipts System) ambao umesaidia wakulima kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ya bei, ubora wa mazao, wizi n.k

Mhe. Kigahe ameeleza kuwa licha ya uchache wa watumishi katika taasisi hii, watumishi wanapaswa kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na kushirikiana na Taasisi nyingine zinazofanya kazi zinzoendana kwani Bodi ndio inayotegemewa na wakulima na wazalishaji wa bidhaa hasa kupitia utaratibu wa stakabadhi ghalani, mfumo ambao umeleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika nchi yetu.

“Ushirikiano ni muhimu kati ya Bodi, Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Soko la Bidhaa na wadau wengine ambapo hii itasaidia kufanikiwa kwa mfumo na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa sasa” Amesema Mhe. Kigahe.

Mhe. Kigahe amesema kuwa taasisi hii inapswa kuongezewa bajeti kwani ina uhitaji mkubwa katika kutekeleza majukumu ya bodi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) Bw.  Asangye Bangu ameeleza kazi mbalimbali zinazofanywa na Bodi hii ambapo amesema kuwa kwa kiasi kikubwa mfumo wa stakabadhi ghalani umesaidia kuweka bei nzuri kwa wakulima, kuanzishwa kwa mifumo ya kitaasisi imara ikiwemo Soko la Bidhaa (commodity exchange) na uimarishaji wa Ushirika, mfumo pia umesaidia kuwezesha wakulima kuwa na akaunti kwenye taasisi za fedha na malipo yote kupitia benki, Mfumo umesaidia kuondoa changamoto ya mizani, vipimo sahihi na ubora kwa kiasi kikubwa.

Aidha ameongeza kuwa bodi imejikita zaid katika matumizi ya TEHAMA ambapo imesaidia Zaidi katika utoaji wa stakabadhi kwa njia ya mtandao, Maombi ya Leseni kwa njia ya mtandao, usajili wa maghala yote nchini na sasa wanajipanga katika kuhakikisha maghala yote nchi yanafungwa mifumo ya CCTV Camera ili kuzuia wizi na kuweka usimamizi mzuri.