Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala

WCF Logo
Serikali Yaendelea Kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Kupitia Mafunzo ya Watendaji
03 Oct, 2025
Serikali Yaendelea Kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala Kupitia Mafunzo ya Watendaji

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala Tarehe 27 Sept, 2025 amehitimisha Mafunzo ya Watendaji wa Stakabadhi za Ghala kwa msimu wa korosho 2025/2026 
Mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 24 Septemba 2025 yamehusisha wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi wanaotarajiwa kuwa watendaji wa ghala kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.

Mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, aliwashukuru washiriki kwa kujitoa na kusisitiza umuhimu wa uadilifu, uwazi na weledi katika kusimamia mfumo huo wa kimkakati.

Kanali Sawala alibainisha kuwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni chachu ya mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kuwezesha biashara ya mazao kufanyika kwa uwazi, kuongeza thamani, kupunguza hasara baada ya mavuno na kuimarisha usalama wa chakula.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeelekeza matumizi ya mifumo rasmi ya mauzo ya mazao ya kilimo kupitia mfumo wa stakabadhi na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX). Hivyo, tunatarajia mkaendeleze uadilifu na maarifa mliyopata ili mfumo huu uwe na manufaa kwa mkulima na taifa kwa ujumla,” alisema Kanali Sawala.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha mfumo wa stakabadhi kwa kuhakikisha maghala yote yanayosajiliwa yanaendeshwa na watendaji wenye ujuzi na uadilifu.